Nguu za Jadi; Maudhui ya Ukabila

Ukabila ni hali ya kupendelea mtu, watu au Jamii fulani kutokana na misingi ya kabila. Upendeleo huu huweza kuhusisha mambo mengi kama vile ajira, elimu, makazi, vyeo, na kadhalika. Katika riwaya hii,

 Wakule ni jamii inayoonyesha ukabila; wao ndio wengi serikalini (uk. 43) kutokana na hali kwamba Mtemi Lesulia ambaye ndiye kiongozi wa nchi ya Matuo anatoka katika jamii hii.

 Wakule wengi hasa walio matajiri wanajibagua na kuishi katika mtaa wa Majuu ambao ni mtaa linamoishi tabaka tawala.

 Kazi za madaraka ziliwaendea Wakule ilhali zile za daraja la chini kama vile kazi za mikono zilifanywa na Waketwa.

 Ukabila unasababisha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kutoka katika jamii ya Waketwa ambao ni wahitimu wa viwango mbalimbali vya elimu na taaluma.

 Siasa za majina zinatawala (uk. 45) na ukabila unafanya watu wasiohitimu katika taaluma mbalimbali kuajiriwa na kusababisha maafa nchini.

 Watu wanaajiriwa kutokana na uchunguzi wa majina yao. Majina yanakuwa kigezo cha kupimia ajira.

 Ukabila unamkolea mtemi kiasi cha kukosa imani ya kuajiri wanajeshi kutoka katika jamii nyingine.

 Dhuluma za Chifu Mshabaha kwa Mangwasha zinatokana na ukabila, anasema"...Waketwa ni watu wasio na akili hata ya kuchagua wachumba." (uk. 20).

 Sagilu anaposema, "Ndege mliolelewa kizimbani nyie hamwezi kuruka. Mtawezaje kuruka ilhali mnaishi mkifikiria kwamba kuruka ni ugonjwa?" haya maneno yanaashiria ukabila. (uk. 176).

 Ukabila unafanya wenyeji wa Matango ambao ni Waketwa kuchomewa nyumba zao na kufurushwa ili wakati wa uchaguzi wa kisiasa wasimpigie mmoja wao kura.

 Mtemi Lesulia anaendeleza hisia za ukabila anapowaita Waketwa panya (uk. 78).

 Kufutwa kazi kwa Mangwasha pia kunatokana na ukabila (uk. 135-137) kwani tunaona anayeajiriwa kuchukua mahali pake ni Mkule.