Maswali na Majibu ya Fasihi Simulizi

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Ikiwa kweli wewe ni mkaza mwanangu,

Nami ndimi nilompa uhai mwana unoringia,

Anokufanya upite ukinitemea mate,

Chakula kuninyima, wajukuu kunikataza ushirika,

Mungu na waone chozi langu, wasikie kilio changu,

Mizimu nawaone uchungu wangu, radhi zao wasiwahi kukupa,

Laana wakumiminie, uje kulizwa mara mia na wanao,

Usiwahi kufurahia hata siku moja pato lao,

Watalokupa likuletee simanzi badala ya furaha,

Wakaza wanao wasikuuguze katika utu uzima wako!

a) Tambua aina ya mazungumzo haya na utoe sababu. (alama 2)

 Maapizo- mhusika anamuomba Mungu kumwadhibu mkaza mwana wake kwa kumpuuza.

b) Eleza sifa mbili za nafsi nenewa. (alama 2)

 Mchoyo- Anamnyima chakula mzazi.

 Mwenye dharau- Anadharau mama mzazi.

c) Taja na ueleze sifa nne za kipera hiki cha fasihi simulizi. (alama 4)

 Hutolewa kwa watu walioenda kinyume.

 Hutolewa kabla ya kula kiapo.

 Yanaweza kutolewa na aliyeathirika.

 Huaminiwa kuwa yataleta maangamizi.

 Hutumia lugha fasaha.

 Hutumia lugha yenye ukali.

d) Unanuia kutumia mbinu ya maandishi kuhifadhi kipera hiki cha fasihi simulizi. Eleza faida na hasara za kutumia mbinu hii. (alama 6)

Faida za maandishi.

 Si rahisi kusahaulika(Data)

 Hufikia vizazi vingi.

 Si ghali.

 Si rahisi data kupotea. Hasara/Udhaifu

 Kiimbo, toni, ishara hupotea.

 Uhai asilia wa fasihi simulizi hupotea.  Watafiti kuandika wanayotaka/wanayohitaji.

 Hadhira hupoteza fursa ya kushirikiana.  Huwafikia tu wanaojua kusoma.

e) Eleza faida tatu na hasara tatu za miviga . (alama 6)

 Huelimisha wanajamii.

 Ni kitambulisho cha jamii.

 Huonyesha matarajio ya jamii kwa vijana.

 Huendeleza na kuhifadhi utamaduni wa jamii.

 Hukuza uzalendo.

 Huhimiza na kukuza umoja wa jamii.

a) Miviga ni nini ? (alama 2)

 Miviga ni sherehe maalum za kitamaduni zinazoambatanishwa na nyimbo na ngoma

b) Fafanua sifa zozote sita za miviga. (alama 12)

 huambatana na utamaduni

 huongozwa na watu maalum

 hufanywa mahali maalum – mwituni

 hufanywa kwa utaratibu maalum

 kuna kula kiapo

 hufanywa wakati maalum - kutawazwa viongozi, harusi, mazishi

 huambatana na mawaidha

 kuna kutolewa kafara zozote

c) Miviga ina majukumu yapi katika jamii ? (alama 6)

 Huburudisha

 Huelimisha

 Huelekeza

 hukuza mila na desturi

 huhifadhi historia ya jamii

 hutambulisha jamii

 huandaa wanajamii kukabiliana na hali ngumu

 njia ya kupitisha maadili kutoka kizazi kimoja hadi kingine

 huonyesha imani za kidini za kijamii

 huonyesha matarajio ya wanajamii

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

Mfalme ana watoto wawili wa kiume na anataka mmoja wao amrithi. Kwa sababu hataki kupendelea yeyote, anawapa changamoto ya kukimbia hadi mji wa mbali kwa farasi wao. Yule ambaye farasi wake atafika mwisho ndiye atakayemrithi. Ndugu hawa wanazembea jangwani kwa siku kadha kwa sababu kila mmoja anataka kufika wa mwisho. Hatimaye wanakutana na mzee mwenye busara ambaye anawapa wosia. Wanapanda farasi upesi na kutoka mbio ili wafike kwenye mji wa mbali walioagizwa na baba yao. Je, Mzee mwenye busara aliwaambia nini?

a) i) Tambua kijipera (alama 1)

Mafumbo

ii) Taja sifa za kijipera hiki (alama 4)

 Limefumba jibu

 Linahitaji mtu kuwaza kwanza ili aweze kubaini fumbo

 Limefumbia juu ya mambo yaliyomo katika jamii-farasi, wana, mfalme

 Ni refu

 Linahitaji mantiki ili kufumbua

 Lina jibu lenye maneno mawili

iii) Wewe ni mmoja wanaowasilishiwa kipera hiki. Taja mambo Matano utakayoyafanya ufanikishe uwasilishaji huu. (alama 5)

 Kushiriki kwa kupiga makofi

 Kuigiza baadhi ya matukio/matendo ya wahusika.

 Kuuliza maswali.

 Hisia/ishara wanazoonyesha usoni huweza kumfanya abadilishe uwasilishaji.

 Kutoa – majibu kwa methali na vitendawili iwapo ngano itamalizikia kwa mtambaji kuwategea vitendawili.

 Kutoa mifano ya baadhi ya wahusika wa utugo kutoka jamii zao iwapo wataulizwa.

 Kutoa funzo katika utungo.

 Kuitikia – mh

 Kucheka/kulia.

 Kujibu maswali.

 Kunyamaza na kusikiliza kwa makini.

b) Soma utungo ufuatao kisha hujibu maswali yanayofuata

Mtoto ni kito mzigo mzito

i. Tambua kijitanzu (alama 1)

Methali

ii. Kipera hiki kinaendelea kudidimia katika jamii yako eleza mbinu tano utakazotumia kukidmisha katika jamii yako. (alama 5)

 Kuirithisha fani yenyewe ya utambaji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

 Kuzihifadhi kwenye maandishi.

 Kukifunza shuleni.

 Kuzitamba mara kwa mara.

 Kukifanyia utafiti ili kubainisha sifa za uwasilishaji wazo na kuzihifadhi.

 Kuzihifadhi kwenye video ili kuhifadhi sifa za uwasilishaji kama vile sauti/kidatu, na miondoko.

 Kutafitia vyanzo vya kudidimia kwazo ili kuvidhibiti/kuvitatua.

 Kuandaa mashindano ya kijipera hiki ili kurithisha utambaji wacho kutoka kizazi hadi kingine/kuwafanya vijana wavutiwe nazo.

 Kufadhili utafiti kuhusu ngano.

 Kushirikisha wageni waalikwa katika ujifunzaji wa kuzifunza kwa mitindo anuwai ili kuwafanya wanafunzi wavutiwe nazo, na kuziendeleza.

 Kuzitumia kufunzia masomo mengine na stadi nyingine kama vile kusikiliza na kuzungumza.

 Kuandaa vipindi vya redio au runinga na kuwaalika mafanani stadi kutamba ili kuwa vielelezo.

 Kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wake.

 Wizara ya elimu kuweka sera zinazohimiza na kulinda utambaji na uhifadhi wake

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

“Kwa taadhima na ruhusa yenu, wapenzi, ninasema hivi: kwamba thawabu ya mja ni sawasawa na jitihada na suna zake. Siku nyingi tumewinda. Na silalamiki kwa kuwa adinasi kwa kawaida huwinda mengi katika sayari hii kwa kadri ya haja na hekima yake. Hana budi, hata hivyo kutumia ubongo wake kwa namna ambavyo Jaliya alivyomkirimu. Naam! Kwa maana wenye hekima hunaswa kwenye hila zao. Nawaomba kwa hivyo mmakinike, pasiwe kwenu faraka bali mhitimu katika nia moja na ushauri mmoja katika ombi letu. Asenteni!”

(a) Tambua kipera hiki. Fafanua jibu lako. (alama 2)

 Kipera hiki ni mawaidha – kuna wosia kwamba kuwepo kwa kumakinika,kuepuka hila, faraka lakini kudumu katika nia moja.

(b) Fafanua muundo wa kipera ulichosoma. (alama 3)

 Utangulizi – huanza kwa kauli ya kuvuta makini ya hadhira – kwa taadhima kuu na ruhusa yenu.

 Mwili – mawaidha huwasilishwa kwa kauli sisitizi pamoja na tamathali za usemi – thawabu ya njia ni sawasawa na jitihada na suna zake. - Adinasi huwinda mengi katika sayari hii kwa kadri ya haja na hekima.

 Hitimisho – Anayeusia huonyesha msimamo wake. Mhitimu katika nia moja na ushauri moja katika ombi letu. Asanteni.

(c) Eleza njia zozote mbili ambazo mtafiti wa kipera hiki anaweza kutumia kukusanya data kukihusu. (alama 4)

 Kunasa sauti/kurekodi

 Kunasa picha na sauti

 Kuandika

 Kushiriki

 Kutazama

 Kutumia hojaji

 Mahojiano

 Kusikiliza

(d) Taja changamoto moja kwa kila mbinu za ukusanyaji data ulizotaja katika swali la c

 Gharama ya utafiti na kunua vifaa

 Mtazamo hasi wa wanajami

 Kudai malipo kutoka wahojiwa

 Uhaba wa mafanani/wazee/wataalamu.

 Vikwazo kutoka kwa watawala

 Ukosefu wa wakati wa kutosha kuwahoji watu.

 Ugumu wa lugha ya mawasiliano

 Ukosefu wa umeme

 Matatizo ya usafiri

(e) Eleza nafasi ya fanani katika fasihi simulizi. (alama 4)

 Huhusika katika uwasilishaji wa haditthi

 Hukusika kwa kutoa kitendawili, kupokea majibu na kuomba mji baada ya mteguaji kukosa jawabu

 Kutunga tungo na kusisimulia/kuziwasilisha

 Kutoa elimu kwa hadhira kwa kuonya kuarifu, kuelekeza, kufahamisha na kukosoa hadhira yake.

 Huendeleza utamaduni wa kupokeza fasihi kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

 Hudumisha na kuendeleza lugha kwa kubuni miundo mbalimbali ya lugha na kuipokea.

 Hushirikisha hadhira katika uwasilishaji wake.

(f) Eleza sifa nne za mwasilishaji bora wa fasihi simulizi. (alama 5)

 Awe na uwezo wa;

kupandisha na kushusha mawimbi ya sauti.

 Matumizi ya miondoko ya mwili za viziada lugha.

 Kushirikisha hadhira

 Matumizi ya maleba

 Aweze kujua hadhira ya na mahitaji yao pamoj na kiwango chao cha elimu.

 Kumudu na kuielewa mazingira ya hadhira yake.

 Kuwa jasiri wa kuzungumza hadharani

 Kujua utamaduni wa hadhira yake.

 Kuwa mfaraguzi – uwezo wa kugeuza kazi ya fasihi papo hapo na kuwasilisha kwa hadhira.

 Kuwa mcheshi.

Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali

1. Angole angole mwanangu

Mwanangu nakuchombeza

Nakuchombeza ulale

Ulale ukiamka

Nikupikie ubwabwa

Na mchuzi wa papa

Ukilia waniliza, wanikumbusha

Ukiwa wa baba na mama

2. Baba na mama watende

Ilimu kunikatizia

Ng’ombe, mbuzi kupokea

Kunioza dumu kongwe

Haliuki na halende

Kazi kupiga matonge

3. Likingia mvunguni

Lavunjavunja vikombe

Likilala kitandani

Languruma kama gombe

a) Bainisha kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)

 Bembelezi / bembea / pembejezi- Unawaliwaza na kuwabembeleza watoto walale auwanyamazewanapolia.

b) Eleza ujumbe unaofumbwa katika wimbo huu. (alama 5)

 Kuhimiza uwajibikaji – nafsi neni kumpikia mwanawe ubwabwa

 Kueleza ugumu wa maisha / umaskini / ukilia wanikumbusha ukiwa wa baba na mama

 Nmafsi neni kukatiziwa elimu – ilimu kunikatizia

 Nafsineni kulazimishiwa ndoa – baba na mama kupokea ng’ombe na mbuzi

 Kuwepo kwa vurugu – lavunjavunja vikombe

 Ukosefu wa usingizi – languruma kama gombe.

c) Tambua mbinu za kifani ambazo zimetumiwa kuwasilisha utungo huu. (alama 3)

 Tashbihi–languruma kama gombe

 Takriri/uradidi–ulale,ukiwa,nakuchombeza,

 Taswira - Languruma kama gombe

 Kinaya – wazazi kumwachisha shule nasfuineni na kumwoza.

d) Bainisha shughuli mojamoja ya kijamii na ya kiuchumi ambazo huendelezwa katika jamii ya utungo huu. (alama 2)

 Kijamii – ndoa – kunioza dume kongwe

 Kiuchumi–ufugaji ;languruma kama gombe

e) Unakusudia kukusanya data kuhusu kipera hiki. Eleza manufaa manne ya kutumia mahojiano. (alama 4)

 Kwa vile mtafiti anakabiliana namhojiwa ana kwa ana ni rahisi kupata habari za ana kwa ana na za kutegemeka.

 Mbinu au sifa za uwasilishaji kama vile; Toni, utendaji, sauti, ishara za uso kubainika kwa mtafiti na hivyo kuimarisha kuelewa kwake.

 Mtafiti anaweza kumfafanulia mhojiwa habari na kuweza kupata data inayoaminika

 Mtafiti anaweza kubadilisha maswali au mtindo wa kuyauliza kulingana na kiwango cha elimu cha mhojiwa; lugha yake mhojiwa na mengine mengi

 Mtafiti anaweza kutambua iwapo mhojiwa anatoa habari zisizo za kweli.

f) Kipera hiki kinazidi kufifia katika jamii yako. Fafanua njia nne ambazo jamii ya kisasa inaweza kutumia kukuza na kuendeleza kipera hiki. (alama 4)

 Jamii inafundisha kipera katika taasisi mbalimbali za elimu kama vile shule ya msingi, vya upili na vyuo vikuu.

 Kuhimiza wataalamu kujihusisha na usomaji na utafiti wa kipera hiki.

 Kuhakikisha kuwa kipera hiki kimepewa nafasi inayostahili katika mfumo wa elimu. kwa mfano kinahusishwa katika tamasha za muziki na drama zinazohusisha taasisi mbalimbali za elimu

 Wanasarakasi wa kisasa wanaendeleza usanii wa kipera hiki.

 Jamii ya kisasa inatumia teknolojia ya habari na mawasiliano k.v Runinga, tarakilishi na redio kuendeleza utendaji wa kipera maathalan kuna vipindi mbalimbali vya watoto nidhazautangazaji

 Watafiti wa fasihi simulizi wanaendelea kukifanyia kipera utafiti, kuandika na kurekodi viperavya fasihisimulizi

 Kipera hiki kinaendelezwa katika jamii za kisasa.

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

“Mwanangu, dunia haitaki papara. Ikiwa unataka kufanikiwa katika mustakabali wako kuwa mtoto mtiifu na mwongofu. Kumbuka kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu…”

a) Tambua na ueleze kipera hiki cha fasihi (alama 2)

 mawaidha

b) Eleza sifa tatu za kipera hiki. (alama 3)

 matumizi mapana ya mbinu za lugha kama vile vile methali

 hutolewa na mzee, mzazi au mtu anayechukuliwa kuwa na hekima

 lugha inayotumiwa huwa ya kipekee inayolengwa kuathiri wanaousiwa

 huweza kufungamanishwa na visa au matukio maalum yanayotokea katika jamii

 huweza kuambatanishwa na mbazi na istiara

c) i) Fafanua dhima tano za kipera hiki katika jamii. (alama5)

 hutoa ushauri kwa walengwa

 Hutoa maelekezo kwa anayepewa mawaidha

 Humtolea mlengwa maonyo asije akapotoka na kutumbukia mashakani

 Humkosoa muathiriwa ambaye huenda alikuwa ameuchukua mkondo usiofaa wa Maisha

 Hutambulisha jamii- kila jamii huwa na aina yake ya mawaidha kulingana na thamani zake

ii) Fanani anawezaje kuihusisha hadhira katika usimulizi wake? (alama 4)

 Kuwauliza maswali

 Kuimba wimbo pamoja na hadhira

 Kuwauliza kukariri jambo alilolisema

 Kuwashirikisha katika vitendo mathalani kupiga makofi au kuigiza wahusika

iii) Eleza utaratibu unaofuatwa wakati wa kutega na kutegua vitendawili. (alama 6)

 Mtegaji hutanguliza kwa kuiambia/ kutangaza vitendawili

 Hadhira hujibu tega

 Mtegaji hutoa kitendawili chenyewe

 Hadhira hupewa muda wa kufikiri na kujaribu kukitegua

 Hadhira ikitoa jibu lisilo sahihi, mtegaji huomba apewe mji ili aweze kutoa jibu

 Mtegaji akipewa mji anaotaka hukubali na kutoa jibu

Niaje wazungu wanaweza kutunza vitu vikajaa kwenye friji. Yani nimeweka soda mbili tu kweyefriji lakini akili haitulii hadi nizinywe. Niko sebuleni nazunguka tu. Najaribu kuwaza vitu vinginelakini wapi akili inaniambia ‘My friend, kunywa soda.’

a) Bainisha kipera cha utungo huu (alama1)

 Kichekesho

b) Fafanua aina tatu za taswira zilizotumika katika kifungu hiki (alama3)

 Taswira ono- kujaa kwenye friji

 Taswira muonjo-kunywa

 Taswira sikivu- inaniambia

 Taswira mwendo-nazungumza tu

c) Utanzu wa kipera hiki huweza kuchukua nafasi muhimu katika fasihi simulizi. Thibitisha kwa hoja zozote sita (alama6)

 Huburudisha watazamaji na waigizaji wenyewe. Burudani hii mara nyingine hupumbaza.

 Huhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii kama vile upashaji tohara, matambiko, majigambo, ngoma, miviga na michezo ya watoto hudumishwa kupitia maigizo.

 Ni kitambulisho cha jamii; kila jamii ina Sanaa ya maigizo ya jamii husika. Miviga na sherehe za arusi na mazishi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.

 Hukuza umoja na ushirikiano wa watu wanapojumuika kushiriki katika maigizo. Hao hujitambulisha kama jamii moja

 Ni nyenzo za kupitisha maarifa na amali za jamii kupitia michezo ya jukwaani. Husawiri mtazamo wa jamii kuhusu masuala mbalimbali kama vile woga, wizi na usaliti.

 Hukuza ubunifu madhalan watoto wanaposhiriki michezo ya watoto, hujifunza kubuni michczo wakiwa wachanga na pia Sanaa ya uigizaji.

 Ni njia ya kuimarisha urafiki. Kwa vile mizaha na utani katika malumbano hukuza urafiki na uhusiano bora

 Huongoza jamii kupambana na mazingira wanamojipata. Kutegemea imani ya wanajamii,matambikoyanaweza kuondoa matatizo katika jarnii kama vile njaa, ugonjwa na ukame kwa kuomba Mungu

 Maigizo huelimisha kupitia maudhui na hulka za waigizaji na kushauri nafsi zao, kuiga au kukashifu hulka hizo.

d) Ufanisi wa uwasilishaji wa utanzu huu unategemea fanani. Teteta kauli hii. (alama5)

 Huwa mchangamfu na mchcshi kwa hadhira yake ili kuwafanya wapcndezwe na hadithi

 Anafahamu utamaduni wajamii yake

 Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na mapendeleo yao. wasichana au wavulana? vijana au wazee?

 Huwa na uwezo wa ufaraguzi - uwezo wa kubadilisha sehemu fulani za sanaa bila kujifunga na muundo asilia.

 Mwenye kumbukumbu nzuri - uwczo wa kukumbuka

 Mwenye uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vyake, uso (ishara-uso) na sauti(kiimbo)

 Mwenye uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo ili kuvuta nadhari ya hadhira yake.

 Hushirikisha hadhira yake katika nyimbo n.k

 Mtambaji hodari na mkwasi wa lugha.

e) Ni changamoto zipi zinaweza kumkabili mwanafasihi mtafiti nyanjani? (alama5)

 Gharama ya utafiti-huenda gharama ikawa kubwa kiasi cha mtafiti kutoimudu. Baadhi ya mafanani au wahojiwa huenda wakadai walipwe kabla ya kutoa habari zozote.hivyo ikiwa mtafiti hana hela basi utafiti wake utakwamizwa.

 Mtazamo hasi wa wanajamii kuhusu ujazaji wa hojaji huenda ukawafanya wengi wao kutojaza hojaji zao. Wanajamii wengine huweza kushuku kwamba mtafiti anawapeleleza na wakakataa kutoa habari.

 Vizingiti vya kidini ambavyo hutokea pale ambapo baadhi ya wahojiwa wanaamini kwamba matendo ya fasihi simulizi k.v matambiko na uimbaji wa taarabu yanaenda kinyume na imani yao ya kidini.

 Uchache wa wazec au wataalamu wa fasihi simulizi ,kukosckana kwa wazee wanaoweza kutamba ngano ama kueleza vipera vingine k.v vitendawili.

 Matatizo ya mawasiliano na uchukuzi ikiwa mkusanyaji analazimika kwenda mbali kukusanya habari,hasa katika sehemu kame itakuwa vigumu iwapo hana gari.

 Ukosefu wa usalama ,huenda mkusanyaji wa fasihi simulizi akavamiwa ,baadhi ya watu si wakarimu na huenda wakamshuku mtafiti na kuvamiwa.

a) Maghani ni nini? (alama 2)

 Mashairi hutolewa kwa kalima badala ya kuimbwa.

b) Eleza sifa za maghani. (alama 6)

 Ni tungo la kishairi. Yaani yana muundo wa ushairi.

 Husimulia matukio kwa kirefu hasa yanayotambwa.

 Hutungwa papo hapo na kusemwa mbele ya hadhira.

 Hutungwa kwa ufundi ukubwa.

 Huweza kutolewa na mtu mmoja au kundi ki watu.

 Anayeghani hujisifu / kusifu kitu / jambo fulani. 

 Huwa na majigambo mengi.  Huambatana na ala mbalimbali za muziki.

c) Fafanua aina zozote tatu za maghani. (alama 6)

 Tondozi – Tungo zinazoghanwa na huwasifu watu, wanyama na vitu.

 Tendi - Huitwa pia ushairi wa ushujaa. Hujumuisha sifa zinazoonyehsa mafanikio ya mashujaa na mbolezi zinazoonyesha anguko la shujaa / mtawala.

 Rara – hadithi fupi na nyepesi za kishairi zinazopitishwa kwa mdomo. Huzungumzia tajriba ya maisha.

 Pembezi – Ni aina ya tondozi inayotolewa kusifu watu fulani pekee mf. viongozi, waganga mashuhuri, waelezi wazuri, wapenzi waliopigania pendo lao n.k.

 Sifo – Ni mashairi ya sifa ambayo hughanwa kumsifu mtu fulani kutokana na matendo yake ya kishujaa

d) Eleza matatizo yoyote sita yanayomkumba mtafiti anapotafiti maghani. (alama 6)

 Kushukiwa kuwa mpelelezi

 Wahojiwa kutoa habari za uongo

 Kutokuwepo wa watu wenye ujuzi wa maghani

 Mila na desturi nyingi kuwa zimeadhiriwa na usasa

 Ukosefu wa fedha za kufanya utafiti

 Maghani kuchukukuliwa kuwa ukale uliopitwa na wakati

Soma utungo ufuatao kasha ujibu maswali

Mimi ni Olichilamgwara

Olichilamgwara mwana mbee wa Ojilong

Ojilong wa Marukatipe

Wazee waliposhindwa

Nilivuka misitu milima na mito

Ni mimi jabali Kipande cha jifya la mama

Nilipokuwa nalisha mifugo

Nilisikia baragumu inalia

Baragumu ya wito

Mifugo wa mtemi wamechukuliwa

Nikachukua mkuki wangu

Wenye kigumba cha mti

Nikachukua upanga wangu

Wenye makali kama mmweso wa radi

Upanga uliopasua pembe za nyati kwa dhoruba moja

Ndipo nilipofyatuka kasi kama umeme

Kufumba kufumbua nikawakaribia nduli

Kusikia vishindi vyangu wakaanza kubabaika

Kuona kifua changu cha manyoya ya kanga wakatetemeka

Macho yangu makali kama kaa la moto yalipowatazama wakakimbia

Mkuki wangu ulipaa kama umeme

Wote wakalala Mifugo wakanifuata…

Mko wapi vijana Mmekuwa kama majivu baada ya moto kuzimika?

a) Tambua kipera ulichokisoma na udhibitishe jibu lako (al. 2)

 Ni majigambo / vivugo  Matumizi ya mimi ni...

b) Tambua sifa za jamii zinazosawiriwa katika utungo huu (al. 2)

 Ni wafugaji – nilipokuwa nalisha mifugo

 Ni wezi wa mifugo – mifugo wa mtemi wamechukuliwa

 Wanajihusisha na vita

c) Kwa kutoa mifano bainisha vipengele vine vya kimtindo vilivyotumiwa na nafsineni (al. 4)

 Istiara (sitiari) Ni mimi Jabali

 Tashbihi – Kasi kama umeme, Ulipaa kama umeme, Kama mmweso wa radi

 Mdokezo – mifugo ikanifuata...

 Swali la balagha – mmekuwa kama majivu baada ya jua moto kuzimika?

 Chuku – upanga kupasua pembe za nyati kwa dhoruba moja

 Msemo – kufumba na kufumbua

 Urudiaji (takriri) nikachukua mkuki wangu, Nikachukua upanga wangu

 Uhuishi – mkuki kupaa

d) Fafanua sifa nne za kipera hiki (al. 4)

 Anayejigamba hutunga kufuatia tukio mahususi katika maisha yake – anakumbuka alivyokomboa mifugo ya Mtemi kutoka kwa wezi

 Huwa na matumizi ya chuku

 Kwa kawaida hutungwa na kughanwa na wanaume

 Hutolewa kwa nafasi ya kwanza m.f Nikachukua mkuki wangu

 Anayejisifu huweza kutaja usuli wake wa kinasaba m.f Ochilamgwara mwana mbee wa Ojilong

 Maudhui makuu ni ushujaa  Hutungwa kwa usanii mkubwa – sitiaru urudiaji tashbihi n.k

e) Eleza mambo manne ambayo mtendaji wa kipera hiki anaweza kufanya ili kufanikisha utendaji wake. (al. 4)

 Avae maleba – mkuki, upanga ngozo

 Atumie kiimbo na toni kupanda na kushuka kwa sauti yake

 Atumie miondoko ya mwili

 Atumie ishara za uso

 Ashirikishe hadhira kwa kuuliza maswali ya balagha

f) Fafanua mikakati ambayo jamii inaweza kutumia ili kuzuia tungo kama hizi kufifia (al. 4)

 Kufanya utafiti Zaidi

 Kuhifadhi kwenye kanda tepu rekodi video n.k

 Kufunza shuleni

 Kupanga mashindano kati ya jamii mbalimbali

 Kuhifadhi katika maandishi

 Kuhimiza watu kutunga tungo kama hizi

 Sherehe mbalimbali

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata

Tumbo: Leo nitakuwa baba na wewe mama. Mimi sipendi mwajificho.

Chausiku: Sawa basi. (Anaimba huku akishika masikio yake) Maskini punda, alinyimwa pembe, akapewa masikio hiyo ndiyo pembe. Pembee pembe, akapewa masikio hiyo ndiyo pembe.

Tumbo: Mamake Chausiku, nahisi njaa. Napeza kula samaki.

Chausiku: Ala! Umejuaje kuwa ninapika samaki? Baba Chausiku, samaki kutoka Soko Mjinga ni tamu kama asali. Chakula ki tayari. (Anampa kitawi chenye vipande vya vijiti). Ndio hii samaki.

Tumbo: (Akiimba) Nimeshiba sana. Asante. Nataka kwenda katika shamba la mahindi kukaza seng’enge. (Anachukua kipande cha mti) Nimechukua nyundo yangu kwenda kujenga ua. (Anatumia kijiti hicho kupigia vijiti vingine ardhini huku akisema kuwa anajenga ua). Chausiku: Nimechoka sasa. Tuimbe kidogo.

Wote: (Wanaimba huku wakirukaruka) Watoto wangu ee! Ee! Mimi mama yenu! Ee! Sina nguvu tena Ee…

a) Bainisha utanzu ambapo utungo wa aina hii unapatikana. (alama 1)

 Maigizo

b) Wewe ni mmoja wa wawasilishaji wa utanzu huu wa fasihi simulizi. Eleza sifa unazofaa kuwa nazo. (alama 5)

 Awe jasiri ili aweze kuigiza mbele ya watu/hadharani.

 Awe na ubunifu ili aweze kufanya uigizaji kuvutia na kuondoa ukinaifu.

 Awe na ujuzi wa kutumia ishara za uso, mwili na miondoko kuonyesha picha ya hali anayoigiza.

 Awe na ujuzi na ufasaha wa lugha ili kuwasilisha mawazo kwa njia mwafaka na inayovutia.

 Aweze kubadilisha toni na kiimbo kulingana na hali tofauti anazoigiza kama vile huzuni.

 Awe na uwezo wa kushirikisha hadhira kwa maswali ya balagha ili kuondoa uchovu.

 Awe na uwezo wa ufaraguzi/ kubadilisha uigizaji wake papo hapo kutegemea hadhira yake na kutoa mifano inayofahamika kutoka katika mazingira ya hadhira.

 Awe anaelewa utamaduni wa hadhira yake ili asitumie maneno na ishara ambazo zinaudhi ama kukinzana na na imani zao.

c) Eleza sifa zozote nne za kipera hiki. (alama 4)

 Waigizaji ni watoto.

 Huhusu shughuli za kiuchumi na kitamaduni kama vile arusi, siasa, ukulima.

 Huandamana na nyimbo za watoto.

 Huwa na miondoko mingi kama vile kujificha, kuruka.

 Huwa na matumizi mengi ya takriri.

 Huchezwa popote.

 Huwa na kanuni fulani.

 Hukoma watoto wakichoka au wakikiuka kanuni

d) Eleza shughuli mbili za kiuchumi zinazodhihirika katika utungo huu. (alama 2)

 Uvuvi – samaki kutoka Soko Mjinga

 Biashara - samaki kutoka Soko Mjinga

 Ukulima – nataka kwenda katika shamba la mahindi

e) Unanuia kufanya utafiti kuhusu kipera hiki. Eleza changamoto zinazoweza kukukabili unapotekeleza shughuli hiyo. (alama 6)

 Gharama ya utafiti kuwa kubwa kiasi cha mtafiti kutoimudu kama vile gharama ya kusafiria na kununulia vifaa.

 Kutojaziwa hojaji kutokana na mtazamo hasi wa jamii dhidi ya ujazaji wake.

 Wanajamii kukataa kutoa habari wakishuku mtafiti anawapeleleza au kwa kuona haya.

 Wanajamii wengine kudai walipwe kabla ya kutoa habari na hivyo kukwamiza utafiti.

 Mbinu nyingine kama vile hojaji huhitaji watu wanaojua kusoma na kuandika na ikiwa mhojiwa hajui utafiti utakwamizwa.

 Uchache wa wazee na wataalamu wa fasihi simulizi kusababisha kukosekana au kupatikana kwa data isiyo ya kutegemewa.

 Utawala kukataa kutoa idhini ya kufanya utafiti.

 Kukosa ufadhili na utafiti kutofanywa kwa kutomudu gharama.

 Muda wa utafiti kutotosha na hivyo kutopata habari za kutosha kuhusiana na mada yake.

 Kikwazo cha mawasiliano ikiwa mtafiti na mhojiwa hawatumii lugha moja na mhojiwa hajui lugha nyingine na kumbidi mtafiti kukodi mkalimani na gharama kuongezeka.

 Ukosefu wa vyombo vya usafiri kunakochelewesha utafiti na kutomalizika katika muda uliopangwa.

 Ukosefu wa usalama kama vile kuvamiwa kwa kushukiwa anapeleleza na kuibiwa vifaa.

 Tatizo la kutafsiri data kutoka lugha za kijamii hadi lugha inayotumika katika utafiti.

 Matatizo ya kibinafsi. Kwa mfano, mtafiti anaweza kushindwa kuidhibiti hadhira yake.

f) Eleza udhaifu wa maandishi kama kifaa cha kuhifadhi data. (alama 2)

 Kuna baadhi ya mambo kama vile kiimbo, toni na ishara ambayo hayawezi kuandikwa kama yalivyowasilishwa na fanani, kwa hivyo hupotea.

 Uhai asilia wa fasihi simulizi hufifishwa na kupotezwa na maandishi.

 Baadhi ya waandishi huenda wakaandika yale wanahitaji kwa wakati mahususi na kupuuza mengine.

 Kuandika fasihi simulizi huifanya kukosa ile taathira asilia kwani kunaipokonya hadhira yake ile fursa ya kushirikiana ana kwa ana na fanani.

 Kuiandika fasihi simulizi huidhibiti na kupunguza hadhira yake na kuathiri vibaya usambazaji wake.

Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.

Malaika Nakupenda malaika x2

Ningekuoa malaika...

Ningekuoa dada...

Nashindwa na mali sina wee...

Ningekuoa malaika x2

Pesa, zasumbua roho yangu x2

Nami niafanyeje, kijana mwenzio

Nashindwa na mali sina wee...

Ningekuoa malaika x2


a) Ainisha wimbo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui. (alama 2)

 Wimbo wa mapenzi

b) Andika sifa mbili za jamii inayosawiriwa na wimbo huu. (alama 2)

 Kuna ushirika wa ndoa

 katika ndoa wanaume hulipa mahali

c) Eleza mikakati sita ambayo mwimbaji angetumia kufanikisha uwasilishaji wa wimbo huu. (alama 6)

 Kutumia sauti inayosikika

 Kutumia miondoko ya mwili na ishara zingine

 Kutumia ala za muziki kama gitaa.

 Kuhusisha hadhira katika uimbaji.

 Kubadilisha toni ya uwasilishaji.

(d) Unanuia kutumia mahojiano kukusanya habari kuhusu nyimbo za aina hii.

I. Eleza manufaa matano ya kutumia mbinu hii. (alama 5)

 Hupata habari za kina

 Sifa za uwasilishaji kama vile toni, ishara za uso na kiimbo hubainika kwa mtafiti.

 Mtafiti anaweza kurekodi majibu ya mhojiwa au kuyaandika.

 Mtafiti anaweza kubadilisha maswali kulingana na kiwango cha mhojiwa.

 Ni rahisi kung’amua wakati unapewa habari ambazo si za kweli.

 Mhojiwa anaweza kumfafanulia mhojiwa maswali.

II. Eleza changamoto tano za kutumia mbinu hii. (alama 5)

 Mbinu hii huhitaji stadi za mawasiliano za juu zaidi.

 Urasmi kutokana na na vikao vya mahojiano huenda ukakatiza mawasiliano kati ya mhoji na mhojiwa.

 Ukosefu wa muda wa kutosha wa mahojiano

 Mhojiwa huenda asimwamini mtafiti.

 Kiwango cha mtafiti cha elimu huenda kikawahofisha wahojiwa.

 Wahojiwa wengine huenda wakampa mtafiti habari za uongo.

Order this full document with more Questions Via WhatsApp Now!