JALADA LA RIWAYA YA CHOZI LA HERI.
Jalada ni sehemu iliyoko juu ya kitabu hasa huwa ngumu na mambo yaliyo muhtasari Wa kile msomaji ataraji ndani.
Jalada huwa kuwili yaani, jalada LA mbele na LA nyuma. Kunavyo vipengele muhimu hasa rangi za michoro na maandishi.
MICHORO.
Kuna michoro ifuatayo kwenye riwaya hii:
MCHORO WA USO.
v Uso upo wa binadamu hasa. Mchoro huu ni wazi kuwa ni wa MTU wa asili ya kiafrika kwani rangi yake ni wazi.
v Wakati mchoro kama huu umetumika, unaashiria undani wa kazi. Ina maana kuwa, ndani mwa riwaya tutarajie kukumbana na wahusika ambao ni waafrika. Japo kwawezatokea wale wa kizungu lakini kiasi finyu sana.
v Mchoro wa kiafrika hivi pia unamaanisha mandhari ya kazi nzima yamesheheni bara la Afrika.
MCHORO WA JICHO.
v Hili ni jicho lililoko kwenye ule uso wa binadamu, hivyo basi ni wazi kama mchana kuwa ni jicho la mtu mwafrika.
v Mbona jicho moja ilhali binadamu wa kawaida anafaa awe na macho mawili?
v Kuna uwezekano mwandishi alilenga sehemu moja ya HERI wala sio SHARI na HERI!
v Hivyo ni wazi hakutaka tuzingatie sehemu ya mateso au matatizo Ila sehemu ya wema, ufanisi, haki ambavyo kwa pamoja vinamwacha mhusika mlengwa akiwa hana budi ila kulia chozi la heri.
KOPE NA NYUZI ZA JICHO.
v Rangi yake ni nyeusi wazi kuwa ni za MTU mwafrika na ni yule wa kawaida asiye na uigaji wowote.
v Jinsi ilivyo kwa nyuzi kuzuia jasho (chungu kama chumvi) kuteremka jichoni ndivyo kijazanda imaanishavyo kuwa mtetezi wa mwafrika ni mwafrika mwenyewe.
v Na pia ilivyo kikawaida kwa kope kuzuia vumbi kuingia machoni, ndivyo ilivyo tena mwafrika kujizuia mwenyewe dhidi ya machafuzi ya hali yoyote aidha ya ndani au nje
CHOZI
v Chozi hilo ndilo CHOZI LA HERI kwani ndani mwake kuna mchoro wa watu watatu wanaoonekana wakicheka.
v Cheko hilo huenda ndilo sababu la CHOZI hili kutoka na kama ni kicheko kisababishi, basi haina tatizo kuamini kuwa ndilo CHOZI LA HERI!
MCHORO WA WATU WATATU.
v Mchoro huo upo kwenye chozi.
v Watu ni watatu ambapo wa kiume ni wawili huku wa kike akiwa peke yake.
v Maana wazi ni kuwa, jinsia zote zimezingatiwa kitabuni isipokuwa jinsia ya kiume imepewa nafasi kuu na kike nafasi ndogo.
v Ikumbukwe kuwa, hali hii inaashiria ubabedume au taasubi ya kiume ambapo wanaume wanapewa nafasi kubwa zaidi ya wale wa kike.
v Hivyo basi, ni vyema sote tutaraji migawanyo ya kijinsia kiwango fulani ndani mwa riwaya.
v Mchoro huo pia unaonyesha wazi kuwa wote wameshikana nyongani kwa ukaribu sana...hii ni ishara kuwa wahusika waafrika ndipo wapate HERI, lazima walikuwa wameSHIRIKIANA na KUUNGANA pamoja kihali na kijinsia.
v Mchoro huo huenda inahalisi kuwa watu hawa watatu ni Umu, Dick na Mwaliko. Walifurahi mno walipokutana wote katika hoteli ya Majaliwa. Riwayani, Umu na Dick walikimbia wote kwa pamoja na wakamkumbatia ndugu yao Mwaliko na huku wakaanza kulia na kutokwa na machozi ya farajaheri.
v Kwa ujumla, michoro kwenye jalada la riwaya ya CHOZI LA HERI ni jazanda ya nini tutaraji ndani mwake
RANGI NA MAANA ZAKE
Kwenye jalada la CHOZI LA HERI kuna rangi hizi;
NYEUSI
v Nyeusi ni ishara ya MTU Wa asili ya kiafrika. Hii ina maana kuwa, mazingira na wahusika ndani ya riwaya Hii ni yenye asili ya Kiafrika.
v Pili, rangi nyeusi inaashiria matatizo au shida. Hivyo basi rangi hii imetiwa jaladani kutudokezea kuwa lazima wahusika kwenye riwaya wanakumbwa na shida au matatizo fulani kwenye safari ya uhusika wao kitabuni.
v Tatu, rangi nyeusi inatumika Kwa maana ya mauti au vifo. Kawaida ya maisha ilivyo ni kwamba, hata mazishini watu huvalia mavazi meusi kama ishara ya maombolezo hasa kuhusiana na kifo. Hali ni hivyo kitabuni kwani wahusika wapo wafao kutokana na sababu mbalimbali.
v Nne, rangi hii yatumika kumaanisha Giza au usiku. Haya ni majira kwenye nyakati za saa hasa baada ya mchana. Jinsi giza au usiku uogopwavyo Kwa maovu na hatari fulani, ndivyo kitabuni tutaraji uoga miongoni mwa wahusika na madhila pia kutendeka hasa majira ya usiku kitabuni.
v Tano, weusi ni ishara ya siri! Siri ni mambo yasiyotamanika kujulikana Kwa watu au kwa wale wasiohusika kwayo. Mara nyingi ni NJAMA au siri tu. Hivyo, tutaraji kukumbana na siri si haba kitabuni baina ya wahusika na njama za hapa na pale!
NYEKUNDU
v Kwanza, huashiria hali ya hatari au onyo! Rangi hii inamaanisha ndani ya riwaya hii tutaraji hatari mbalimbali pamoja na onyo kadha wa kadha. Wale wameanza au wamekisoma hiki kitabu mtabaini kuwa Bw. Ridhaa, analazimika kutoka kwao na jamaa yake kutokana na vitisho na hatari ya kupoteza uhai hata akawa amepoteza mkewe, wanawe na mkazamwana.
v Pili, ina maana ya damu au ngeu. Kitabuni kuna uhusiano wa kinasaba au kiukoo ambayo sote twajua ni uhusiano wa KIDAMU! Zaidi, kuna umwagikaji wa damu...watu wanauawa hasa kwa ghasia zitokanazo na siasa.
v Tatu, rangi hii pia inaashiria mapenzi. Riwayani, yapo mapenzi ya huba yapelekeayo wahusika kadha wa kadha kuoana. Pia, kunao wanaoonyesha au kudhihirisha mapenzi kwa kushirikiana na kusaidia wenzao kwa hali mbalimbali.
NYEUPE
v Kwanza, ina maana ya AMANI! Tunataraji kitabuni kudumu amani aidha kabla au baada ya hali fulani. Ni kweli na wazi kwamba hakuwezekani kuwapo na CHOZI LA HERI bila AMANI kuwepo miongoni mwa wafurahiao.
v Pili, humaanisha hali sawa au shwari. Hivi ni kumaanisha eti hali hata kama yaweza kuwa mbaya vipi kitabuni lazima tutaraji wema, utulivu na hali shwari aidha kabla au baada ya hali mbaya au ya machafuko. Licha ya mambo kuwaendea vibaya wahusika wengi riwayani, hatimaye mna amani ya kudumu.
UDHURUNGI.
v Hii rangi inatumika mara nyingi kumaanisha utajiri au ubwanyenye. Hali wazi kweli kitabuni lazima mna wale washikilia vyombo vya uchumi pamoja na wenye kumiliki vijasiriamali. Hao ni matajiri ambao utajiri wao na maisha yao ndio ukweli wa rangi hii, UTAJIRI!
MANJANO.
v Ina maana ya TUMAINI. Jinsi wengi tujuavyo huwa na hiyo maana ya tumaini au Kitabuni, japo wahusika wana pitia mateso matatizo na bali mbaya, kupo wahusika watakaokuwa na ari ya kuona kesho yao njema licha ya kuwa hali mbaya wakati huo. Tumaini hili, ndio uti wa mgongo wa kuona kesho Leo na kuipangia wema hata kama Leo hio ni mbaya.
v Jina lake mwandishi liko maeneo yayo hayo na limeandikwa kwa rangi ya manjano. Rangi hii pia huashira ukomavu. Mwandishi wa riwaya hii ni mwenye tajriba pana. Amekomaa katika uandishi wa kazi za fasihi. Masuala anayoyaangazia ni yale yanayoiathiri jamii yake. Ametumia mtindo unaoashiria upeo wa ukomavu wake.
KIJANI KIBICHI
v Maana ya rangi hii ni uhai na rutuba. Riwayani yamo maeneo yaliyo na rutuba yanayotoa mazao mengi. Katika eneo la Msitu wa Heri alikoishi Ridhaa kwa miongo mitano, mwanzoni kulikuwa kama jangwa la Kalahari lakini Ridhaa alihakikisha kuwa kijiji hiki kimepata maji ya mabomba hadi eneo zima likatwaa rangi ya chanikiwiti. Miti mingi kama Miambakofi, mivule na miti mingine kapandwa. Maeneo mengine yaliyokuwa na rutuba ni kama Msitu wa Mamba. Watu waliogura makwao walipohamia hapa walikata miti na kupanda vyakula kama mahindi ambayo yalifanya vizuri mno.
SAMAWATI
v Buluu.Sote twajua kuwa rangi hii ni ya mbingu (SKY) ila, rangi yake hutokea kwenye sura ya maji hasa ziwa au bahari! Ujumla, twaita rangi yake maji samawati...na hii ina maana kuwa maji ni uhai. Sina shaka, hakuwezi kuwapo wahusika bila wao kuwa na uhai...hii ndio maana nzima ya kukubali kwamba, uhai upo kitabuni kwani jinzi tu tulivyoaanza na rangi nyeusi(kifo) hakuna kifo bila uhai kutanguliza!