Maudhui ya Nafasi ya Mwanamke katika jamii
Haya ni maudhui yanayonyesha namna mwanamke amesawiriwa katika tamthilia ya Bembea ya Maisha.
Mwanamke amesawiriwa kama mwerevu na mwenye maarifa, hekima na busara. Kwa mfano, katika uk. 6 Kiwa anasema kuwa Sara amebarikiwa na watoto wenye akili nzuri. Wote wamehitimu vizuri na kuleta faraja. Tunaona Neema amesoma na kuhitimu Chuo kikuu na ana kazi nzuri. Asna na Salome vilevile wamefanikiwa kusoma hadi Chuo kikuu. Salome alipita mtihani kwa kupatafirst class. Alibahatika kwenda nwambo kuendeleza masomo yake
¾
Mwanamke anaonekana kama mzazi anayestahili kujifungua watoto wa kike na wakiume na hasa watoto wa kiume. Asipopata watoto wa kiume, anasutwa na kukejeliwa.
¾
Tunaelezwa kwamba Sara alisutwa na kutukanwa na wanajamii kwa kukosa mtoto wa kiume hata baada ya kujaliwa na mabinti watatu baada ya muda mrefu bila watoto (uk. 6,7).
¾
Mwanamke amesawiriwa kama mtu mvumilivu na anayestahili kuvumilia
mateso na bughudha za ndoa. Kwa mfano, Sara anavumilia ndoa yake ambayo ilikuwa na changamoto nyingi. Aidha anavumilia mumewe Yona baada ya kumtesa na kumchapa kichapo cha mbwa. Neema anapewa mawaidha na mama yake kuhusu kuzidi kuvumilia ndoa yake. Kudhihirisha suala hili la uvumilivu wa ndoa tunamwona Neema akimweleza mumewe kwamba anakubaliana na wazo kuwa hawaishi katika ndoa ya raha mustarehe mia fil mia (uk. 48). Wazo hili linaonyesha kuwa Neema pia anavumilia ndoa yake na Bunju.
¾
Mwanamke ameonyeshwa kama mtu anayestahili kujukumika katika majukumu ya nyumbani. Anasawiriwa kama mtu mwenye majukumu ya shambani, jikoni na nyumbani kwa jumla. Yona anapomkuta Sara ameketi, analalamika kuwa hajaandaliwa chochote. Inambidi Sara amtumie salamu Dina ili aje amsaidie kupika. Hali hii inaonyesha kuwa ni jukumu la mwanamke kupika na kuandaa chakula kwa mumewe.
¾
Kizazi cha jana kimemsawiri mwanamke kama mtu asiyestahili kupata elimu. Sara anasema kuwa siku zao elimu ya wasichana ilifanywa bezo. Yeye aliachia darasa la saba (uk. 33).
¾
Mwanamke amesawiriwa kama kiumbe dhaifu. Kiumbe ambacho hakifai kushindana na mwanamume. Sara anamwambia bintiye Neema kuwa utamaduni ungali una nguvu na hawezi kushindana na mwanamume (uk. 66).
¾
Wanawake katika tamthilia hii wameonyeshwa kama watu wenye msimamo dhabiti. Sara na binti zake wamesawiriwa kama wenye msimamo imara. Kwa mfano, Sara anasimama na familia yake hata baada ya kutukanwa na kukejeliwa na wanajamii. Hakuwacha familia yake, alisimama nayo hadi wakati wa mwisho. Asna pia ana msimamo wake kuhusu ndoa (uk. 53). Anashikilia msimamo kuwa ndoa ni taasisi inayomkandamiza mwanamke na kuwa haifai.