Nguu za Jadi; Maudhui ya Ufisadi

Ufisadi umejitokeza kwa njia mbalimbali kupitia kwa baadhi ya wahusika na unachukua sehemu kubwa katika riwaya hii.

 Serikali ya Mtemi Lesulia inawaajiri watu wasiokuwa na ujuzi wala maarifa huku walio na uwezo huo wakiachwa (uk. 44). Tunaambiwa ajira zinatolewa kibubusa na kwa kujuana hasa katika misingi ya ukabila.

 Taasisi na mashirika ya serikali yanamilikiwa na mitandao ya wezi na hivyo kuipoka nchi hadhi yake (uk. 47). Rasilimali ya nchi inafujwa na watu walioshabikia wizi.

 Polisi nao wanaendeleza ufisadi pale wanapowatoza madereva wa Lonare faini zisizoeleweka; pale Lonare anapohangaishwa na polisi kwa makosa madogomadogo; kupokonywa leseni, na kadhalika.

 Maudhui ya ufisadi yanajitokeza pale kundi la mabwanyenye linapohujumu dhamana na hawala za serikali.

 Upokeaji hongo unaonekana pale watu waliotumwa kumkatizia Lonare maisha walipomjia na kumwonyesha pesa walizopewa na maadui zake ili kumuua.

 Kitendo cha Sagilu kujaribu kumhonga Mangwasha kwa pesa ili afaidi penzi lake pia ni kitendo cha ufisadi (uk. 60).

 Kauli ya Mtemi Lesulia ya kuamuru jalada la ardhi ya Matango kufichwa inadhihirisha ufisadi (uk. 78). Alitaka kuwaondoa Waketwa wasimpigie kura Lonare au Mbaji wakamshinda yeye au Sagilu.

 Nanzia na Mbwashu wamiliki ardhi hiyo huku wakisema ardhi hiyo ilikuwa imetengewa ujenzi wa soko. Hivi vyote vinaashiria ufisadi.

 Ufisadi unaonekana pale Sagilu na Sihaba wanapojaribu kumshawishi Mbaji kwa kila njia ili asimfanyie Lonare kazi (uk. 98).

 Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa na mtemi na jamaa yake pamoja na marafiki zake wanapojaribu kuwapoka Waketwa ardhi ya Matango kwa njia zisizo halali.

 Hongo inatolewa kwa Chifu Mshabaha, Sagilu na Sihaba kutoka kwa Mtemi Lesulia katika mchakato wa kuwanyan’ganya Waketwa ardhi yao ya Matango.

 Kitendo cha kuwachomea wenyeji wa Matango nyumba na kuwafurusha kinatokana na ufisadi kwani kuna vijana waliohongwa kutekeleza uhalifu huo.

 Maudhui ya ufisadi pia yanaendelezwa na taasisi ya magereza kwani tunaona milango ya gereza ikifunguliwa ili wahalifu kama vile Sihaba watoke (uk. 85).

 Ufisadi pia unaendelezwa kupitia wahusika kama vile Mbwashu na Sagilu wanaotumia njia haramu kuagiza bidhaa ghushi nchini na kukataa kulipa ushuru mbali na kutoa mlungula bidhaa hizo ziliposhikwa na maafisa wa forodha (uk. 68).

 Tashbihi inayotolewa ya kumlinganisha Mtemi Lesulia na mjusikafiri juu ya kichuguu inapiga mwangwi ufisadi uliokuwepo katika serikali yake (uk. 93). Utawala wake unafisidi pato la nchi linalotokana na jasho la raia wake.

 Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa pia na mwanasheria Mafamba. Huyu anashiriki ufisadi pale anapoficha siri za watawala kwa kutoa habari za uongo mbele ya korti kuhusu vyeti ghushi vya ardhi iliyomilikiwa na wenyeji wa Matango.  Ufichuzi wa mwanasheria Mwamba unaweka bayana ufisadi unaohusishwa na ardhi ya Matango (uk. 95).

 Mrima anapokea mlungula kutoka kwa Sagilu ili kuhujumu kampeni ya Lonare na kumuunga mkono Mtemi Lesulia (uk. 105-114).

 Ufisadi unabainika Lonare anapomwambia Sagilu, "Nimekuja kukukabidhi mlungula huu uliokuwa umempa Mrima." (uk. 116).

 Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa na mhusika Ngoswe anaposhiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya ambazo 'zilisambazwa nchini kwa siri' (uk. 123).

 Kupitia kwa Mashauri pia, ufisadi unaendelezwa pale anaposhirikiana na Sagilu kufisidi vipusa na meno ya ndovu (uk. 127).  Ufisadi unayawezesha mashtaka yaliyofikishwa kortini kuzimwa hata kabla ya kesi kuanza.

 Mtemi na Sagilu wanatumia vishawishi vya pesa kuwahonga vijana ili wazue vurugu na kuharibu kura za mpinzani wa Sagilu katika eneo la Matango (uk. 128).