Utabaka ni hali inayosababisha jamii kujibagua katika makundi hasa mawili; matajiri na maskini au wenye mali na vyeo na wasio navyo.
Kuna tabaka la juu linalohusisha wakwasi, matajiri na wakuu wa serikali ambao pia wamejitenga na kuishi katika mtaa wa kifahari uitwao Majuu (uk. 7 na uk. 51).
Wananchi wa kawaida wanaishi katika mitaa ya matabaka ya chini na yale ya kati kama vile Majengo, Matango na Majaani na wale wa tabaka la juu kama Mtemi na wakule wakubwa serikalini wanaishi mtaa wa Majuu.
Tunaarifiwa nchi ya Matuo ilishikilia utabaka (uk. 45), "...matajiri wakawa wenye nchi na wananchi wakasalia kuwa wana wa nchi".
Tabaka la juu la akina Mtemi Lesulia, Sagilu, Nanzia, Mbwashu, hata Ngoswe ndilo lililomiliki nyenzo za uzalishaji mali na ndilo lililohujumu dhamana na hawala za serikali.
Mangwasha anashangaa kumwona Mbwashu akiwasili pale kanisani kwa gari aina ya Land Rover kumaanisha kwamba hadhi yake haimruhusu kutumia gari kama lile, kwa kawaida yeye hutumia gari la kifahari la Lexus. Cheiya anatamani maisha ya kifahari kutokana na utabaka uliokuwepo. Anafanya usuhuba na Mashauri anayeishi mtaa wa Majuu naye akapata kuishi huko (uk. 118).
Kisa cha mfalme wa Ufaransa na malkia wake kwenye karne ya 18 kinaashiria utabaka pale raia waliishi katika umaskini huku tabaka la mfalme likiishi maisha ya kitajiri (uk. 148-149).